News

Posted On:: Aug, 05 2024
News Images

Naibu Waziri wa Utamaduni wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma amesema anafurahi kuiona tasnia ya Sanaa ikiheshimiwa na kuthaminiwa katika kipindi hiki baada ya jitihada mbalimbali zilizofanywa na Serikali na wadau binafsi kuhakikisha sekta hiyo inawanufaisha wasanii nchini.

Mhe. Mwinjuma akiwa miongoni mwa wasanii walioshuhudia vipindi mbalimbali vya mageuzi ya tasnia hiyo hapa nchini ameelezea moja ya jitihada zake na uthubutu aliouchukua, yeye na msanii mwenzake kipindi cha nyuma wa kufungua kesi ya madai na kupata ushindi dhidi ya kampuni iliyotumia kazi zao za sanaa bila wao kuhusishwa ilivyoleta mabadiliko makubwa kwenye Sekta hiyo nchini.

Mhe Mwinjuma ameyasema hayo Agosti 2 2024 jijini Dar es salaam alipokua akizungumza na wasanii kwenye mkutano wa utoaji wa elimu ya fedha kwa wasanii ‘Sanaa Pesa Summit’

“Miaka kadhaa nyuma mimi na mwenzangu tuliamua kufungua kesi ya madai dhidi ya Kampuni moja iliyotumia kazi yetu bila sisi kuhusishwa. Kwa wakati ule ilionekana ni jambo gumu kushitaki kwa sababu ya matumizi ya kazi ya sanaa bila ridhaa kwani sanaa ilikuwa haionekani kuwa na thamani”

“Nina furaha leo kuona baada ya kupambana kwa muda mrefu na kushinda kesi ile mambo makubwa yalifanyika nchini ikiwemo sheria ya Hakimiliki na Hakishiriki namba 7 ya Mwaka 1999 iliyofanyiwa marekebisho na kuruhusu kesi za hakimiliki kufunguliwa katika mahakama yoyote yenye uwezo wa kusikiliza tofauti na awali ambapo ilisikilizwa mahakama ya Wilaya pekee jambo ambalo linalowapa uhuru wasanii kuchagua mahakama ya kufungua mashauri yao” Ameeleza Mhe. Mhe. Mwinjuma

Amefafanua kuwa katika kipindi hiki wasanii wameamka; kazi zao zinapotumika bila ridhaa zao wamekuwa wakifungua kesi za madai na kushinda.