News

Posted On:: Dec, 05 2024
News Images

Klabu za Simba, Yanga na Azam za Ligi kuu ya Tanzania Bara zimepata fursa ya kucheza mechi za kirafiki na Klabu za Ligi kuu ya Urusi pamoja na kuweka kambi kwa timu hizo katika kipindi cha mapumziko ya ligi kuu.

Fursa hiyo imepatikana kufuatia ziara ya Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro nchini humo ambapo alikutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Michezo wa nchi hiyo Mhe. Mikhail Degtyarev Desemba 3, 2024.

Pamoja na fursa hiyo Mhe. Ndumbaro amependekeza kuwapo na ushirikiano wa kubadilishana utaalamu katika ngazi ya vilabu pamoja na kuwa na michezo ya mara kwa mara ya kirafiki baina ya vilabu vya ligi mbalimbali za nchi hizo mbili.

Aidha, Waziri Ndumbaro ametembelea ofisi za Bodi ya Ligi Kuu ya Urusi na kufanya mazungumzo na Mkurugenzi Muendeshaji Mkuu wa bodi hiyo Bw. Evgeniy Melezhikov ambapo wamekubaliana kuanzisha ushirikiano baina ya timu za taifa na kuwa na mechi za kirafiki.