News

Posted On:: Mar, 19 2024
News Images

Serikali imesaini Mkataba wenye thamani ya shilingi Bilioni 286 na kampuni ya China Construction Engineering Group (CRCEG) kwa ajili ya ujenzi wa uwanja mpya wa mpira wa miguu Mkoani Arusha.

Akizungumza wakati wa hafla ya kusaini Mkataba huo leo Machi 19, 2024 Jijini Dar es Salaam, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Damas Ndumbaro amesema uwanja huo utakuwa na uwezo wa kuingiza watazamaji 30,000 huku akibainisha kuwa uwanja huo utakuwa wa kisasa zaidi Afrika Mashariki.

Amesema Serikali itahakikisha ujenzi huo unafanywa kwa haraka kwa kuwa Tanzania itakuwa mwenyeji wa michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON) mwaka 2027 ikiwa ni juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Amesema uwanja huo utachagiza kwa kiasi kikubwa utalii nchini kwa kuwa uwepo wa uwanja huo utakuwa chachu shughuli mbalimbali tofauti na mpira wa miguu kama vile mchezo wa riadha, biashara zitakazokuwa zinafanyika.

"Uwanja huu utakuwa na ubora wa hali ya juu kwani utakuwa na vyumba vya watu mashuhuri, tumefanya zoezi hili leo ambapo, Rais Samia wetu anatimiza miaka mitatu ya uongozi wake, amesema Dkt. Ndumbaro.

Aidha, ameipongeza Kamati ya kudumu ya Bunge ya Elimu Utamaduni na Michezo kwa juhudi ilizofanya za kuhakikisha zoezi hilo.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Elimu, Utamaduni na Michezo Mhe. Husna Sekiboko amemtaka Mkandarasi wa uwanja huo ahakikishe kuwa ujenzi huo unakamilika kabla ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.

"Wakandarasi hakikisheni kabla ya uchaguzi wa mwaka 2025 uwanja uwe umefikia kiwango kinachoridhisha na utekelezaji huo uanze haraka iwezekanavyo ikiwa ni maandalizi kuelekea katika michuano ya Mataifa ya Afrika (AFCON),"amesema.

Amesema Kamati itatoa ushirikiano kuhakikisha ujenzi huo unafanyika kama ilivyokusudiwa akibainisha kuwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anaitendea haki sekta ya michezo kama anavyofanya kwenye sekta nyingine akitoa wito kwa wakazi wa Arusha watunze miundombinu ya uwanja huo.

Wakati huo huo Mkuu wa Mkoa wa Arusha Mhe. John Mongela amesema uwanja huo utaongeza idadi ya Watalii katika Mkoa huo.

"Tunaahidi kuenzi ujenzi huo, tutahakikisha unajengwa usiku na mchana ili usiweze kukwama kwa upande wetu, tuweweka historia kubwa."