News

Posted On:: Dec, 23 2024
News Images

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Palamagamba Kabudi amesema serikali inatambua mchango mkubwa wa wadau wa sekta ya habari katika kukuza maendeleo ya taifa, kuimarisha uwazi, na kuhamasisha uwajibikaji.

Mhe. Prof. Kabudi amesema hayo leo Desemba 18, 2024 jijini Dar es Salaam katika mkutano na wadau wa sekta ya habari na utangazaji, ambao amekutana nao kwa lengo la kufahamiana na kushirikiana kutatua changamoto za sekta ya habari.

“Serikali inatambua mchango mkubwa wa wadau wa sekta ya habari katika kukuza maendeleo ya taifa, kuimarisha uwazi, na kuhamasisha uwajibikaji. Ili kufanikisha malengo haya, serikali inatarajia Waandishi wa Habari na vyombo vya habari kuzingatia kikamilifu maadili ya taaluma yao. Hii inajumuisha kuonyesha uadilifu, uwazi, na kuepuka kusambaza habari za upotoshaji, uchochezi, au zinazoweza kuhatarisha amani na usalama wa taifa,” amesema Mhe. Prof. Kabudi.

Ameendelea kusema kuwa, vyombo vya habari vinapaswa kuwekeza katika ubunifu, teknolojia za kisasa, na mikakati endelevu ya kibiashara, ili kuongeza ufanisi wa shughuli za vyombo vya habari na kuimarisha uhimilivu wa kiuchumi wa sekta ya habari kwa muda mrefu.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa amesema sekta ya habari imeendelea kukua kutokana na mazingira wezeshi yaliyowekwa na Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Hadi sasa Tanzania inajivunia kuwa na magazeti 179, majarida 174, vituo vya redio 247, vyombo vya habari vya mtandaoni 355 na vituo vya televisheni 68, kwa ujumla vyombo vya habari vilivyosajiliwa nchini vinakadiriwa kufikia 1,023. Aidha vyombo hivyo vimefanikiwa kuajiri zaidi ya Waandishi wa Habari 2,000, wakitoa mchango mkubwa katika sekta ya habari na mawasiliano,” amesema Msigwa.

Amesema, kumekuwa na mabadiliko chanya katika kipindi cha hivi karibuni, ikiwemo marekebisho ya baadhi ya sheria na kanuni za habari, pamoja na juhudi za kufungua milango ya mazungumzo kati ya serikali na wadau na kuimarisha ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi.

“Haya yote ni matokeo ya dhamira njema ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika kuhakikisha sekta ya habari inapata nafasi ya kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya nchi yetu,” amefafanua Msigwa.