News
Nikiwa Msemaji wa Serikali ninalo jukumu la msingi la kuhakikisha kunakuwa na sio tu mawasiliano bali mawasiliano ya karibu na yenye tija kati ya Serikali na wananchi, Serikali yetu na wadau mbalimbali wa ndani na nje ya nchi wakiwemo taasisi, nchi mbalimbali, viongozi na hata makundi mbalimbali kwa maslahi ya Taifa letu na kwa kuzingatia Sheria, kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali. Jukumu hili linajumuisha pia kutoa majibu na ufafanuzi wa masuala mbalimbali ambayo yanahitaji kujibiwa na Serikali.
HALI YA UTENDAJI WA BANDARI
# Katika kipindi cha mwezi Mei 2024 hadi Novemba 2024, kiwango cha shehena kilichohudumiwa na bandari zote zilizo chini ya Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) ni tani milioni 16.5 ambayo ni ongezeko la asilimia 5.92 ya shehena ya tani milioni 15.6 iliyohudumiwa katika kipindi kama hiki mwaka uliopita (Mei 2023 hadi Novemba 2023).
# Tumepata mafanikio makubwa pia kwa upande wa idadi ya Makasha yaliyohudumiwa na bandari zote zilizo chini ya TPA katika kipindi cha Mei 2024 hadi Novemba 2024 ambapo takwimu zinaonesha kuwa tumehudumia makasha 621,584 sawa na ongezeko la asimilia 3.29 ikilinganishwa na makasha 601,805 yaliyohudumiwa katika mwaka uliopita (Mei 2023 hadi Novemba 2023).
# Katika kipindi cha mwezi Mei, 2024 hadi Novemba 2024, kiwango cha shehena kilichohudumiwa na Bandari ya Dar es Salaam ni tani milioni 14.4 ambayo ni sawa na ongezeko la asilimia 5.6 ikilinganishwa na shehena ya tani milioni 13.7 iliyohudumiwa katika kipindi kama hiki mwaka uliopita (Mei 2023 hadi Novemba 2023).
# Tangu kampuni hii ya “DP WORLD DAR ES SALAAM” ianze uendeshaji wa shughuli za bandari mwezi Aprili 2024, mafanikio mbalimbali yamepatikana kama ifuatavyo; kwa mujibu wa mkataba, Kampuni ya DPW inapaswa kuwekeza Dola za Kimarekani milioni 250 (TZS bilioni 675) katika kipindi cha miaka mitano. Katika kipindi cha miezi mitano tayari wameshawekeza TZS 214.425 bilioni (31%) kwa ajili ya manunuzi ya mitambo ya kisasa; ukarabati wa mitambo iliyokuwa ya TPA; na usanifu na usimikaji wa mfumo wa TEHAMA wa kisasa wa uendeshaji wa Bandari.
# Wastani wa muda wa meli kusubiri umepungua kutoka siku 46 mwezi Mei 2024 hadi kufikia wastani wa siku saba (7) ikiwa ni siku 0 kwa meli za makasha; siku 12 kwa meli za kichele; na siku 10 kwa meli za mizingo mchanganyiko.
# Kutokana na matumizi ya vitendea kazi vya kisasa (SSG na RTG) katika kupakia na kushusha mizigo, muda wa kuhudumia meli za makasha gatini umepungua kutoka wastani wa siku saba (7) hadi wastani wa siku tatu (3) hivyo kupunguza idadi ya meli zinazosubiri kutoka wastani wa meli 35 mwezi Septemba 2023 hadi wastani wa meli 15 mwezi Septemba 2024.
# Katika kipindi cha miezi mitano gharama za matumizi ya uendeshaji wa bandari zimepungua hadi kufikia asilimia 2.7 ya makusanyo wakati ambapo matumizi yalikuwa yanaongezeka kwa asilimia 15.1 kwa mwezi kabla ya kukabidhiwa uendeshaji wa bandari kwa kampuni ya DP WORLD DAR ES SALAAM.
# Katika kipindi cha miezi mitano (Aprili hadi Septemba 2024) tangu DPW Dar es Salaam waanze kuendesha Gati 0-7 katika Bandari ya Dar es Salaam, Serikali imeshakusanya jumla ya shilingi bilioni 325.3 ikiwa ni mapato yanayotokana na shughuli za mikataba iliyoingiwa kati ya TPA na DP World, ikijumuisha tozo ya pango (land rent), tozo ya mrabaha (royalty), na Ardhi (warfage).
UTOAJI WA HUDUMA ZA TRENI
# Toka kuanza kwa safari za treni ya umeme kati ya Dar, Moro na Dodoma, Juni 14, 2024 na kuzinduliwa kwa safari ya “Mchongoko’’ Novemba 1, 2024, huduma zetu zimeendelea kuboreka na kwa sasa jumla ya ruti kumi (10) ambazo ni ruti nne (4) kutoka Dar es Salaam – Dodoma, Dodoma - Dar es Salaam pamoja na ruti mbili (2) kati ya Dar es Salaam - Morogoro.
# Hadi kufikia mwisho wa mwezi Novemba makusanyo yalikuwa ni shilingi bilioni 30 na idadi ya abiria waliosafirishwa mpaka Desemba 11, 2024 ni abiria 1,174,404, na hii ni kwa kipindi cha miezi minne tangu kuzinduliwa kwa njia za treni ya umeme kati ya Dar es Salaam na Dodoma mwezi Juni 2024 idadi ambayo ni mara mbili ya abiria waliosafirishwa na treni ya zamani (MGR), ambayo ilisafirisha jumla ya abiria 400,000 katika kipindi cha mwaka mmoja.
# Kuhusu ukamilishaji wa ujenzi wa reli katika awamu zilizobaki Makutopora - Tabora - Isaka – Wakandarasi wapo uwandani na wanaendelea na kazi na tunatarajia kukamilisha ujenzi wa vipande vilivyobaki mwaka 2028.
MRADI WA USAFIRI WA HARAKA WA MABASI (BUS RAPID TRANSIT-BRT)
# Mradi wa Usafiri wa Haraka wa Mabasi (Bus Rapid Transit (BRT)) ulibuniwa mwaka 2004 chini ya Halmashauri ya Jiji kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari barabarani Jijini Dar es Salaam. Aidha, gharama ya ujenzi wa miundombinu ya Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka kwa awamu zote sita inagharimu kiasi ya fedha za Marekani dola milioni 1,079.54 (Sawa na zaidi ya shilingi Trilioni 2.5).
#Utekelezaji wa mradi wa BRT umepata mafanikio kadhaa ikiwa ni pamoja na uboreshaji wa huduma ya usafiri wa umma Dar es Salaam na kukuza ajira; kupunguza msongamano wa magari; kupunguza gharama za isafiri; kukuza sekta binafsi na uwekezaji wa imma kwa njia ya ibia (PPP); kukuza matumizi ya teknolojia ya kisasa; kuthibiti upotevu wa mapato ya nauli kwenye mfumo pamoja na kupunguza uchafuzi wa mazingira.
HALI YA UPATIKANAJI WA PEMBEJEO NCHINI
# Makadirio ya mahitaji ya mbolea na visaidizi vyake kwa msimu wa 2024/25 ni tani 1,000,000 ambapo hali ya upatikanaji wa mbolea nchini kufikia tarehe 30 Novemba, 2024 ulikuwa ni tani 769,060 sawa na asilimia 77 ya mahitaji. Kiasi hicho cha upatikanaji kilitokana na bakaa ya msimu uliopita tani 260,403, uzalishaji wa ndani tani 58,669 na zilizoingizwa kutoka nje ya nchi tani 449,988.
# Uzalishaji wa ndani wa mbolea umeendelea kuimarika kutokana na jitihada zinazofanywa na Serikali kwa kushirikiana na Sekta Binafsi kwa kutumia malighafi za ndani ikiwemo rock phosphate ambapo uzalishaji wa ndani wa mbolea umeongezeka kutoka tani 84,696 mwaka 2022/2023 hadi tani 158,628 msimu wa 2023/2024.
# Makadirio ya mahitaji ya mbegu bora nchini kwa msimu wa 2024/2025 ni tani 80,000 ambapo upatikanaji umefikia tani 42,471.09 sawa na asilimia 53 ya makadirio ya mahitaji. Kati ya hizo, tani 29,819.57 zimezalishwa ndani ya nchi na tani 12,651.52 zimeingizwa kutoka nje ya nchi.
# Katika msimu wa 2024/2025, Serikali inatekeleza Mpango wa utoaji wa Ruzuku ya Mbolea na mbegu bora za mahindi kwa wakulima. Lengo la utoaji wa ruzuku hiyo ni kupunguza gharama ya mbolea kwa mkulima ili kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo, kuimarisha usalama wa chakula na kuongeza upatikanaji wa malighafi za viwanda.
# Utaratibu wa utoaji wa ruzuku unatumia mfumo wa kidigitali wa Digital Subsidy System ambao unaratibiwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (Tanzania Fertilizer Regulatory Authority – TFRA) na Taasisi ya Kuthibiti Ubora wa Mbegu Tanzania (Tanzania Official Seed Certification Institute – TOSCI). Utoaji wa ruzuku unazingatia mahitaji halisi ya mkulima kulingana na taarifa za usajili na bajeti ya Serikali iliyotengwa.
USAFIRI WA ANGA
# Mpaka sasa kampuni ya ndege Tanzania ina ndege zifuatazo;-
* Boeing 767 – 300F (Mizigo) 1
* Boeing 737 – 9 Max 2
* Boeing 787 – 8 (Dreamliner) 3
* Airbus 220 – 300 4
* DE Havilland Q400 5
# Ndege hizi zinafanya safari katika vituo 27, ambapo 15 ni vituo vya ndani ya nchi (Mikoa) pia vituo vya nje ya nchi ikiwemo (Africa (9), Nje ya Afrika (3) - Dubai, Mumbai na Guangzhou)
# Katika kipindi cha kutoka Januari mpaka Desemba 17, 2024, ATCL imefanikiwa kusafirisha abiria 1,109,803, mizigo tani 10,181 na kufanya safari za ndani na nje ya nchi 16,522
# Usalama na Utendaji; ATCL ina vibali vya usalama wa kufanya safari katika vituo takribani 12 vya nje ya nchi.
#Ufufuaji wa ATCL umesaidia kukuza sekta mbalimbali ikiwemo utalii kwa kutangaza vivutio vyetu na kuwawezesha watalii kufikia vivutio hivyo.