News
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Prof. Palamagamba
Kabudi, amelipongeza Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) kwa hatua ya kuunganisha Mfumo wa wadau wa Sanaa (AMIS) na Mfumo wa TAUSI na kiagiza kuwa Mfumo huo uzinduliwe na
kuanza kazi mara moja.
Prof. Kabudi amesema hayo katika kikao cha kupokea Wasilisho kuhusu kuunganishwa kwa mifumo hiyo, Desemba 18, 2024 jijini Dar es Salaam ambapo amesema, hizo ni jitihada kubwa za kutekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, ya kuboresha mifumo ya Serikali ili iweze kusomana na kufanya kazi kwa ufanisi.
Kwa Upande wake Naibu Waziri wa wizara hiyo, Mhe. Hamis Mwinjuma, ametoa pongezi kwa BASATA kwa kazi yao kubwa ya kuboresha mazingira ya kazi kwa wadau wa sanaa na wasanii nchini, ambapo ameeleza kuwa hatua hiyo ni ya kihistoria katika maendeleo ya sekta ya sanaa.
Kikao hicho kilihudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, na Msemaji Mkuu wa Serikali Ndg. Gerson Msigwa, Katibu Mtendaji wa BASATA, Dkt. Kedmond Mapana, Mwenyekiti wa Bodi ya BASATA, pamoja na watendaji wengine wa wizara.