News

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Barani Afrika (CAF), Patrice Motsepe amesema amekoshwa na maandalizi ya miundombinu ya viwanja ikiwemo Benjamin Mkapa kuelekea mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wachezaji wa Ndani (CHAN).
Kauli hiyo ameitoa tarehe 19 Desemba, 2024 alipofanya ziara yake nchini kwa kutembelea Uwanja wa Benjamin Mkapa na kushuhudia uboreshaji wa miundombinu yake.
Tanzania inatarajiwa kuwa Mwenyeji wa mashindano ya CHAN yatakayofanyika Februari mwakani kwa kushirikiana na nchi za Afrika Mashariki Kenya na Uganda.
Rais huyo alitoa wito kwa wadhamini kujitokeza kudhamini soka ili kutoa mchango kwa vijana wa mataifa yao.
“Wito kwa taasisi binafsi kutoa sapoti katika soka, Tanzania kuna vijana wanafanya vizuri ambao wanapeperusha bendera ya taifa kama vijana chini ya umri miaka 15 waliotoka kuchukua ubingwa wa mashindano ya shule (African Schools Fotball Championship).“CHAN inakwenda kuwafungua milango watu wengi hasa vijana na watoto kutimiza ndoto zao katika mashindano,“alisema Motsepe.
Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali Ndg. Gerson Msigwa amesema wamefurahi kuona Rais wa CAF, Motsepe ameridhishwa na maandalizi ya CHAN.
Amesema uwanja huo umefikia asilimia 70, jambo kubwa lililobaki ni zoezi la kubadilisha viti elfu 60 ambalo hadi mwisho wa mwezi litakamilika.
“Kama serikali tumefurahi kuona Rais wa CAF ameridhishwa na miundombinu ya maandalizi ya CHAN hasa uwanja wa Benjamin Mkapa.“Tumemwambia kuwa kutakuwa na viwanja vitatu vya kufanyia mazoezi yaani Gymkhana, Chuo cha Sheria na Meja Jenerali Isamuhyo uliopo Mbweni, Dar es Salaam" amesisitiza Msigwa.