News

Posted On:: Dec, 05 2024
News Images

Waziri wa Utamaduni Sanaa na Michezo Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Michezo wa Urusi Mhe. Mikhail Degtyarev na kujadiliana masuala mbalimbali ya ushirikiano kwenye sekta ya michezo baina ya nchi hizo.

Viongozi hao wamekutana Desemba 3, 2024 katika ofisi za Wizara hiyo, Jijini Moscow ambapo moja ya mambo waliyojadili ni juu ya ushirikiano kati ya Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya na Chuo Kikuu cha Moscow pamoja na Chuo Kikuu cha St. Petersburg katika kubadilishana ujuzi na utalaamu kwenye sekta hiyo.

Akizungumza wakati wa kikao hicho Mhe. Ndumbaro ameeleza kuwa, Tanzania inahitaji utaalamu zaidi hususani kwenye eneo la matibabu kwa wanamichezo, walimu wa michezo ya soka, judo, mitupo, kurusha tufe na miruko ambapo Urusi imepiga hatua katika maeneo hayo.

Mhe. Ndumbaro amefafanua zaidi kuwa, wataalamu hao watasaidia mikakati ya Serikali kuelekea mashindano ya AFCON 2027 na yale ya Olimpiki 2028.

Kwa sasa chuo cha maendeleo ya michezo Malya kinaendelea na ujenzi wa kituo cha umahiri katika michezo ambapo ushirikiano huo utaongeza tija kwa kituo hicho kinachojengwa na serikali ya awamu ya sita .

Waziri Ndumbaro yupo nchini Urusi kwa ziara ya kikazi katika sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo ambapo ameendelea kukutana na viongozi na wadau mbalimbali nchini Urusi kwa ajili ya kutafuta fursa kwa wadau wa sekta anazozisimamia.