News
Wizara, Taasisi, Mashirika, wakala za Serikali zimetakiwa kutenga Bajeti ya kutosha kwa ajili ya kushiriki Michezo ya Wizara, Idara na Taasisi za Serikali (SHIMIWI) ili kukidhi malengo na misingi ya kuanzishwa kwa michezo hiyo na kuleta tija.
Agizo hilo limetolewa na Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Doto Biteko wakati akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kufungua mashindano ya 38 ya SHIMIWI yanayoendelea Mkoani Morogoro ambapo amesema, hatopenda kusikia visingizio vya aina yoyote kutoka kwa wale wasiotuma washiriki.
“Kama tumekubaliana kufanya jambo lazima tulifanye jambo linakuwa ni lazima siyo hiari, kama kuna sababu ya kuliboresha tuboreshe kwa kufanya mabadiliko na siyo kukubaliana bila kufanya utekelezaji” amesema Dkt. Biteko.
Agizo la Dkt. Biteko linafuatia kushuka kwa idadi ya vilabu vinavyoshiriki mashindano hayo kutoka 74 mwaka 2023 hadi 66 mwaka 2024 jambo ambalo amesema linaashiria kuwepo kwa changamoto katika uendeshaji wa michezo ya SHIMIWI na hivyo kuwaagiza waajiri na Wakuu wa Taasisi ambao hawakutuma washiriki kutoa maelezo juu ya uamuzi wao kwa ajili ya hatua siku zijazo.
Amesema Mashindano ya aina hiyo mbali na kuwauganisha watumishi, lakini yanawezesha mshikamano miongoni mwao na kujenga afya ambayo ndio msingi w utendaji bora wa kazi na wenye tija.
Kwa Upande wa Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma ameishukuru Serikali chini ya Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendeleza sekta ya michezo na kusema kwa sasa kuna mafanikio makubwa kitaifa na kimataifa yaliyofikiwa katika sekta ya michezo nchini.
Katika tukio hilo ambalo Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo Bw. Methusela Ntonda ameshiriki, Naibu Waziri Mwinjuma amesema, Wizara itaendelea kufanya kazi kwa bidii kuhakikishaTanzania inaendelea katika michezo mbalimbali sambamba na kuibua na kuonesha vipaji ficho miongoni mwa wanamichezo.
Awali Mwenyekiti wa SHIMIWI Daniel Mwalusamba amesema lengo la michezo hiyo pamoja na kuimaridha afya, kufahamiana na kubadilishana uzoefu, inawajenga watumishi katika misingi ya uzalendo, kujitolea kulipa kodi, na usikivu kwa serikali iliyoko madarakani.
Mashindano ya SHIMIWI mwaka 2024 yamebebwa na Kauliimbiu “Michezo huoengeza utendaji kazi, Shiriki uchaguzi Serikali za Mitaa kwa ujenzi wa Taifa Endelevu.