News

Posted On:: Feb, 22 2024
News Images

Katibu Mkuu Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Gerson Msigwa amesema kuwa Wizara hiyo itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta binafsi ili kufanikisha matukio mbalimbali yenye maudhui yanayoitangaza Tanzania na kukuza uchumi kupitia Sekta ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Katibu Mkuu Msigwa ameyasema hayo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi cha viongozi wa Wizara na Wakuu wa Taasisi zilizo chini ya Wizara hiyo na wadau wa Sanaa kutoka Sekta binafsi wanaotambulika kama “Sanaa Sounds” ambapo pamoja na mambo mengine viongozi hao wamejadiliana juu ya ujio wa Tamasha la Serengeti Music Festival 2024 ambalo limekuwa likifanyika hapa nchini.

Amesema lengo la kukutana na kushirikisha wadau hao ni kuhakikisha kuwa ujio wa Tamasha hilo unapewa nguvu zaidi na Tamasha hilo linafanyika kwa viwango vya juu zaidi kwa kufanya maboresho na kulipa hadhi ya kuwa Tamasha kubwa la Sanaa na burudani linaloitangaza Tanzania Kimataifa ikilinganishwa na yaliyopita.

“Tumeshirikisha Sekta binafsi ili watupe mbinu bora ya kuliandaa Tamasha hili na kutafuta wadhamini. Tunataka liwe tamasha kubwa nchi nzima linalohusu muziki, wadau wawe tayari tushirikiane kuikuza Sanaa yetu kulikuza Tamasha hili Kimataifa, naamini itawezekana”, amesema Katibu Mkuu Gerson Msigwa.

Aidha Katibu Mkuu Msigwa amesema wameamua kushirikiana na wadau hao wa Sanaa kwa kuwa wameonesha uwezo mkubwa hasa katika maandalizi ya matamasha mbalimbali na pia kupata wadhamini kitu ambacho awali kilitazamwa kama changamoto katika kulikuza tamasha hilo na kulitangaza Kimataifa.

Kwa upande wake Beatrice Ndungú ambaye ni mwakilishi wa Kampuni hiyo akizungumza mara baada kufanya mawasilisho mbalimbali amesema wana uzoefu wa kufanya shughuli mbalimbali ambazo zimekuwa na mafanikio makubwa ikiwemo uandaaji wa Tuzo za Muziki Tanzania zilizofanyika mwaka 2023 Jijini Dar es Salaam.

“Tumejadiliana juu ya kuona namna ambavyo Sanaa inaweza kusaidia kukuza utamaduni, tuna imani ya kuwa na matokeo makubwa na kupitia Tamasha hili tutachangia kuikuza Sanaa ndani na nje ya Tanzania”, amesisitiza Beatrice.