News

Posted On:: Sep, 15 2024
News Images

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe Hamis Mwinjuma ametoa rai kwa vyombo vya Ulinzi na Usalama kuendeleza programu za kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana katika michezo ikiwamo kuwa na mpango maalumu wa kuwatafuta vijana wanamichezo wenye vipaji na sifa za kujiunga na majeshi ili wakati wote timu zijazwe na damu changa.Rai hiyo ameitoa Septemba 15 2024 katika ufungaji wa Michezo ya Majeshi Tanzania (BAMMATA 2024) tukio ambalo limefanyika katika uwanja wa Jamhuri mkoani Morogoro.

Aidha Mhe. Mwnjuma amesisitiza vyombo hivyo kuendelea kushirikiana na Wizara yenye dhamana ya Michezo kuweka taratibu ambazo zitawezesha majeshi kuendelea kutoa wachezaji bora walio na uwezo wa kuwakilisha kimichezo kitaifa na kimataifa.

Mhe. Mwinjuma alipata nafasi ya kutoa zawadi kwa washindi katika mashindano hayo yaliyofanyika kwa muda wa wiki nzima yakishirikisha michezo mbalimbali kutoka vyombo vya ulinzi na usalama vya nchi ambapo amesema mashindano hayo yanakuza ushirikiano.

"Ni dhahiri kwamba mashindano haya yamethibitisha dhamira, umahiri na weledi wa Majeshi yetu katika kukuza na kuendeleza sekta ya michezo nchini, tumeona madhumuni ya mashindano haya ni kukuza ushirikiano na mshikamano jambo ambalo limefanikiwa kwa kiwango kikubwa" amesema Mhe. Mwinjuma