News
Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma ametoa rai kwa Halmashauri, Wilaya na Mikoa ambayo haijaguswa na miradi ya AFCON 2027 zianze kuunga mkono jitihada za Serikali kwa kujenga viwanja vya kisasa vya michezo ili pia zipate vyanzo vipya vya makusanyo ya maduhuli katika maeneo yao.
Mhe. Mwinjuma ametoa rai hiyo leo Septemba 3 2024 bungeni jijini Dodoma alipokua akijibu swali la mbunge wa viti maalumu Mhe. Jacqueline Kainja aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kujenga viwanja vya michezo nchini katika ngazi ya wilaya.
Mhe. Mwinjuma amesema jukumu la ujenzi wa miundombinu ya michezo ni la Serikali kwa kushirikiana na wadau wa sekta ya michezo zikiwemo Taasisi, mashirika, watu binafsi na mamlaka za Serikali za Mitaa.
Ameeleza kuwa katika kuhakikisha kila Wilaya inakuwa na viwanja vya michezo Serikali inaendelea kuzihimiza Mamlaka za Mitaa kutenga mafungu katika bajeti zao ili kutekeleza miradi ya ujenzi wa viwanja vya michezo katika maeneo yao.
Mhe. Mwinjuma ameongeza kuwa tayari kuna halmashuari zimeanza utekelezaji huo ambazo ni Kinondoni (Uwanja wa KMC Stadium), Bukoba Mjini (Uwanja wa Kaitaba), Nyamagana (Uwanja wa Nyamagana) na Namungo (Majaliwa Stadium).
Aidha, amebainisha kuwa Halmashauri ya Wang’ing’ombe inajenga Kijiji cha Michezo kitakachokuwa na viwanja vya michezo ya soka, mpira wa pete, Netiboli, na Mpira wa kikapu.