News

Posted On:: Jul, 18 2024
News Images

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Suleiman Serera amelipongeza Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Umoja wa Mataifa (UNESCO)

kwa kuendelea kushirikiana na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo kupitia Kituo chake cha Urithi na Ukombozi wa Bara la Afrika kilichoko Jijini Dar es Salaam katika kuhifadhi urithi unaoshikika na ule usioshikika wa utamaduni na ukombozi nchini Tanzania.

Dkt. Serera ametoa shukrani hizo Julai 17, 2023 Jijini Dar es salaam wakati wa kikao kazi cha awali kati ya Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Afrika cha Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na UNESCO kujadili uandaaji wa makala maalum ya maeneo ya historia ya ukombozi yaliyopo nchini Tanzania ambayo itasaidia kutoa elimu kwa jamii kuhusu mchango wa Tanzania katika harakati za kuzisaidia nchi za Afrika kupata uhuru.

Akizungumza wakati wa kikao hicho, kilichohudhuriwa na Mkurugenzi Mkazi wa UNESCO nchini Tanzania, Michel Toto, wataalamu kutoka Wizara ya Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Tume ya Taifa ya UNESCO na Maafisa wa UNESCO, Dkt. Serera amelishukuru shirika hilo kwa kuitambua lugha ya Kiswahili kama lugha ya Kimataifa na kuipa heshima ya siku maalum ya kuadhimishwa.

Amesema Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo itaendelea kushirikiana na UNESCO katika uendelezaji wa maeneo mbalimbali yakiwemo ya uendelezaji na ukuzaji wa lugha ya Kiswahili Duniani pamoja na uhifadhi wa historia ya mchango wa Tanzania katika ukombozi wa Afrika ili kizazi cha sasa na kijacho kiweze kujifunza kuhusu historia hiyo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa UNESCO nchini Tanzania Bw. Michel Toto amesema Shirika hilo liko tayari kushirikiana na Kituo cha Urithi na Ukombozi wa Bara la Afrika katika kuhifadhi na kuendeleza urithi wa ukombozi katika nyanja mbalimbali.

Aidha, Mkurugenzi huyo ameridhia ombi lililowasilishwa na Wizara kupitia Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika la kusaidia kuhifadhi kumbukumbu na nyaraka mbalimbali za maeneo ya historia ya ukombozi kidigiti.