News

Posted On:: Jun, 07 2024
News Images

Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Dkt Damas Ndumbaro amesema Serikali ina mikakati mbalimbali ya kuwezesha wadau kuwekeza katika kuzalisha vipaji vya michezo hususani mpira wa miguu pamoja na kuandaa miongozo na kanuni mahususi zinazowalinda wadau wanaoanzisha shule maalumu za kukuza na kuendeleza vipaji vya michezo ili kuhakikisha wananufaishwa na uwekezaji wanaoufanya.

Dkt. Ndumbaro ametoa kauli hiyo leo Juni 7 2024 Bungeni jijini Dodoma wakati akijibu swali la Mbunge wa viti maaalumu Norah Waziri Mzeru aliyetaka kujua mpango wa Serikali wa kuwawezesha wadau wa michezo kuwekeza katika kuzalisha vipaji vya michezo mbalimbali hasa mpira wa miguu.

Mhe. Dkt Ndumbaro ameongeza kuwa Serikali imeendelea kuwaunganisha wadau hao na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) kupitia programu kadhaa za kuibua na kuendeleza vipaji zikiwemo UMITASHUMTA,UMISETA na UMISAVUTA.

Aidha Dkt. Ndumbaro ameongeza kuwa Serikali imeanzisha mafunzo ya elimu ya michezo ngazi za Astashahada na Stashahada katika vyuo sita (6) nchini vikiwemo, vyuo vya ualimu Butimba, Korogwe, Mpwapwa, Monduli na Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya.

Fauka ya hayo, Serikali inaendelea kuimarisha utoaji wa mafunzo ya Shahada ya kwanza katika elimu ya michezo kwenye Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kwa lengo la kuongeza idadi ya wataalamu wa kufundisha michezo ili kupunguza gharama za uwekezaji.