News

Posted On:: Nov, 06 2024
News Images

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Hamis Mwinjuma ahimiza kuendelea kuimarishwa Ushirikiano kati ya Tanzania na China katika Sekta ya Utamaduni na Sanaa ili kurahisisha mawasiliano baina ya Mataifa haya mawili na kuinua vipaji vya wasanii.

Mhe. Mwinjuma amesema hayo wakati aliposhiriki Kikao cha viongozi wa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Watu wa China kilichofanyika tarehe 4 Novemba, 2024 ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya miaka 60 ya ushirikiano wa kidiplomasia na mwaka wa Utamaduni na Utalii kati ya China na Tanzania.

Aidha, amesisitiza kuanza kwa mchakato wa Ujenzi wa Jumba Changamani la Utamaduni Jijini Dodoma ili kuonesha utajiri na uanuwai wa Urithi wa Utamaduni wa Taifa letu, Kuwajengea uwezo Wataalam wa Utamaduni na Sanaa nchini China na Ubidhaishaji wa Lugha ya Kiswahili nchini China na Uimarishaji mafunzo ya Lugha ya Kichina nchini Tanzania.

Nae, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo Bw. Methusela Ntonda amesisitiza umuhimu wa China na Tanzania kuendelea kushirikiana zaidi katika miaka 60 ijayo ambapo alifafanua kuwa ushirikiano wa Tanzania na China katika Sekta ya Utamaduni na Sanaa utasaidia kujenga utangamano na kurahisisha mawasiliano baina ya Mataifa haya mawili.