News

Posted On:: Nov, 30 2023
News Images

Washiriki wa Tamasha la World Happy Deaf Family Festival 2023 wametembelea Hifadhi ya Taifa ya Mikumi mkoani Morogoro Novemba 27, 2023 kujionea vivutio adhimu vya Wanyamapori.

Akizungumza mara baada ya ziara hiyo ndani ya Hifadhi ya Mikumi, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Sanaa nchini na Mkuu wa msafara huo Dkt. Emmanuel Ishengoma amesema ziara hiyo ni utekelezaji wa maagizo ya Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ambayo aliyatoa Januari 22, 2022 ambapo alizielekeza Wizara za Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na Maliasili na Utalii kuunganisha matukio yao katika sekta za Utamaduni, Sanaa na Michezo kimkakati ili kutangaza utalii wa Tanzania.

“Kwa hiyo hawa waliofika hapa Mikumi leo kutoka nchi 43, kila bara hapa limewakilishwa, baada ya kumaliza mashindano, sisi Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo na Bodi ya Utalii Tanzania tumekuja hapa kuendendeleza hiyo dhana ya Rais ya kutumia matukio yote ya Wizara kutangaza nchi yetu na utalii wetu” amesema Dkt. Ishengoma.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Miss na Mr Deaf International (MMDI) Bi.Bonita Ann Leek kutoka nchini Marekani Bi. Bonita Leek amesema mwaka jana 2022 waliichagua Tanzania kuja kufanya mashindano hayo na kukubaliana tena mwaka 2023 mashindano hayo yafanyike tena Tanzania kwa kuwa yalifana sana na kuamua kurudi tena mwaka huu.

“Nimefurahia Tanzania kuwa na mbuga kama hii, nimeona Wanyama tofauti tofauti na jambo hili litasaidia viziwi wengine duniani nao kuvutiwa na kutembelea Tanzania” amesema Bi. Bonita.

Naye Kaimu Meneja wa Habari na Uhusiano Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) Bw. Robert Mwasunya amesema ujio wa walimbwende, watanashati na wanamitindi kutoka jamii ya watu wenye chanamoto ya usikivu duniani unaendelea kukuza Sanaa kwenye sekta ya utalii duniani watakaporudi kwenye nchi zao watatangaza utalii wa Tanzania kupitia picha walizopiga katika Hifadhi ya Taifa ya Mikumi na kuzirusha kwenye mitandao mbalimbali duniani ikiwa ni mkakakati wa bodi hiyo kukuza utalii wa ndani, kikanda na kimataifa.

Wakiwa katika hifadhi hiyo washiriki hao wameshuhudia makundi ya Wanyamapori wakiwemo simba, twiga, tembo, nyati, nyumbu na swala chini ya uratibu wa Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Tamasha hilo limehusisha washiriki zaidi ya 160 kutoka mataifa ya Afrika Kusini, Australia, Belarus, Brazil, Ethiopia, Falme za Kiarabu, Guyana, Haiti, Hispania, India, Iran, Italia, Kenya, Kongo DRC, Malasia, Macedonia, Marekani, Mexico, Misri, Morocco, Msumbiji, Nigeria, Pakistan, Poland, Romania, Rwanda, Senegal, Siera Leone, Sudan Kusini, Thailand, Tunisia, Jamhuri ya Czechoslovakia, Ufaransa, Uganda, Ujerumani, Ukraine, Urusi, Zambia, Zimbabwe na wenyeji Tanzania.