News

Posted On:: Jul, 18 2024
News Images

Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma amesema Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo itaendelea kutekeleza maono ya Mhe. Rais Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kuhusu uendelezaji wa michezo kwa kuvifuata vipaji vya michezo kwenye ngazi za chini.

Mhe. Mwinjuma ametoa kauli hiyo mkoani Shinyanga alipozindua rasmi Ligi ya Dkt. Samia/ Katambi Cup ambayo imelenga kuibua vipaji vya Vijana ambayo inashirikisha timu 32 za mpira wa miguu iliyoandaliwa na Mbunge wa Shinyanga Mjini, Mhe. Patrobas Katambi.

Mhe. Mwinjuma amesema katika kipindi cha nyuma hakukuwa na utaratibu rasmi wa kutengeneza vipaji na kuvilea huku akibainisha kuwa sasa fursa ya kufanya hivyo ni kubwa kutokana na maono makubwa aliyonayo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt Samia Suluhu Hassan kwenye eneo la Michezo

“Rais wetu Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan anapenda michezo hivyo hatua ya Mhe. Katambi kuanzisha ligi hii ni kumuunga mkono Mhe. Rais katika kukuza michezo hapa nchini na kutoa ajira kwa vijana,” amesema Mhe. Mwinjuma na kuongeza kuwa kazi ya Wizara ni kutengeneza daraja kwa kuweka uwanja sawa kati ya vijana wa Shinynga na wa Ilala au Arusha na yeyote mwenye kipaji atawezeshwa ili kipaji chake kitumike katika ngazi kubwa zaidi ikiwemo vilabu na timu za Taifa.

Kuhusu zawadi watakazopewa washindi wa ligi kwenye ligi hiyo amesema mshindi wa kwanza atapewa shilingi milioni 6 pamoja na kombe,mpira na jezi huku mshindi wa pili akipewa shilingi milioni 3, kombe, mpira na jezi na mshindi wa tatu atapewa shilingi milioni moja, mpira na jezi.