Habari
MUZIKI WA SINGELI KUINGIA KWENYE ORODHA YA URITHI WA DUNIA

Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo ipo katika hatua za mwisho za kukamilisha orodha ya Kitaifa ya Urithi wa Utamaduni Usioshikika ikiwa ni hatua ya kukamilisha mchakato wa Uteuzi wa Muziki wa Singeli kwenye orodha ya kimataifa ya UNESCO.
Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Ndg. Methusela Ntonda, Agosti 19, 2025, jijini Dar es Salaam, alipofungua mkutano wa wadau wa utamaduni walioshiriki kuandaa oridha hiyo.
Ntonda amewataka washiriki kutumia kikao hicho kufanya maboresho ya mwisho ya nyaraka za orodha ya kitaifa ya urithi huo, ikiwemo muziki wa singeli kabla ya orodha hiyo kuwekwa rasmi kwenye tovuti za Wizara.
Hatua hiyo itaharakisha uteuzi wa vipengele vya urithi wa utamaduni kwa kunazingatia matakwa ya Mkataba wa UNESCO wa mwaka 2003, hususani Ibara ya 11 na 12.
Aidha, ameelekeza utekelezaji wa mpango uliopo wa kuwa na vipengele mbalimbali vya Urithi wa Utamaduni ili kuorodheshwa kimataifa ikiwemo: Michoro ya Tingatinga, Sanaa za Kimakonde, Taarabu, Tambiko la Waluguru, Falsafa za Mwenge wa Uhuru, Tamasha la Mwakakogwa (Zanzibar), Tamasha la Bulabo (Wasukuma), Ngoma ya Msewe na kilimo cha kontua (Mbinga-Ruvuma)
Kikao hicho kimejumuisha washiriki kutoka UNESCO, Tume ya Taifa ya UNESCO-Tanzania, Maafisa Utamaduni wa Wizara kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, wawakilishi wa sekta binafsi, NGOs pamoja na wawakilishi wa jamii kutoka mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Pwani.