Habari
TANZANIA NA ZIMBABWE KUENDELEA KUSHIRIKIANA KIUCHUMI KUPITIA RASILIMALI ZAKE

Tanzania na Zimbabwe zimekubaliana kushirikiana katika kuimarisha uchumi wa mataifa hayo, kupitia rasilimali zilizopo zikiwa na historia ya kushirikiana tangu enzi za kupigania uhuru wa mataifa hayo.
Hayo yameelezwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Zimbabwe Mhe. Kanali Mstaafu, Kembo Campbell Mohadi, alipofanya ziara katika Kituo cha Urithi wa Ukombozi wa Bara la Afrika jijini Dar es Salaam Agosti 31, 2025.
Mhe. Mohadi alisema, Tanzania na Zimbabwe zina kila sababu ya kushirikiana kwakua zina historia ya undugu wa kisiasa ulioleta ukombozi kwa mataifa hayo na mengine katika ukanda wa kusini mwa Afrika.
"Sisi Zimbabwe tunaishukuru Tanzania kwa namna ilivyotusaidia wakati tunadai uhuru wetu, tutaendeleza ushirikiano huu wa kihistoria ulioasisiwa na Baba wa Taifa hili Mwalimu Julius Nyerere" alisema Mhe. Mohadi.
Katika ziara hiyo, Mhe. Mohadi aliweka shada la maua katika majina ya Wanajeshi wa Kitanzania waliojitoa maisha yao kuisaidia nchi ya Zimbabwe kupata uhuru pamoja na kuzungumza na wazee ambao walikuwa sehemu ya kamati ya ukombozi wa nchi hiyo.
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Ndg. Methusela Ntonda, ambaye alishiriki ziara huyo alisema, ziara hiyo inatokana na mchango wa Tanzania wa hali na mali pamoja na kuhifadhi historia ya ukombozi wa nchi hiyo kupitia wapigania uhuru ambao waliishi hapa nchini.
Naye Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni, Bw. Boniface Kadili alisema, ni heshima kubwa kwa Tanzania kutambuliwa kama kitovu cha kusaidia wapigania uhuru walioshiriki harakati za ukombozi kutoka nchi za Kusini mwa Afrika vikiwemo vyama vya ZANU na ZAPU vya nchini Zimbabwe.
Ameongezea kuwa, mbali na kituo hicho kuwa makumbusho ya kumbukumbu za historia barani Afrika, lakini pia ni utambulisho na fahari kwa Waafrika ambapo alisema kituo kitandelea kuhifadhi na kutunza kumbukumbu kwa faida ya vizazi vya sasa na baadae.