Habari
TANZANIA YATIA SAINI MKATABA WA NCHI MWENYEJI WA SEKRETARIETI YA BARAZA LA MICHEZO LA UMOJA WA AFRIKA KANDA YA 4

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imesaini mkataba wa makubaliano ya nchi mwenyeji na Baraza la Michezo la Umoja wa Afrika Kanda ya 4 (AUSC Region 4) kuwa makao makuu ya Sektretarieti ya kanda hiyo kufuatia ushindi uliopata baada ya kupigiwa kura na wanachama wa kanda hiyo mnamo Mei 5, 2023 kwenye Mkutano wa Kwanza wa Kanda hiyo jijini Arusha.
Tanzania ilichaguliwa kufuatia utayari wake katika kuendeleza sekta ya michezo ikiwemo ujenzi wa miundombinu, uibuaji na uendelezaji wa vipaji pamoja na uanzishaji wa programu za michezo kwa vijana kushirikiana na nchi wanachama.
Mhe. Kabudi amesema ni wakati huu ambapo Tanzania kwa kushirikiana na nchi wanachama imeendelea kusuka ajenda mbalimbali za michezo duniani na kupelekea kupewa uwenyeji wa mashindano ya CHAN na AFCON miongoni mwa nchi wanachama wa kanda hiyo.
"Tunashukuru kwa kuichagua Tanzania kuwa mwenyeji wa sektretarieti ya kanda yetu hii, na kupitia mkataba tuliosaini tunaahidi kutekeleza yale yote yaliyopo ndani ya mkataba kwa manufaa ya maendeleo ya michezo ndani na nje ya nchi zetu.
Kwa upande wake Mratibu wa Kanda hiyo, Ndg. Decius Chipande ameishukuru Tanzania kwa ushirikiano inayotoa kwa kanda hiyo katika kuibua fursa zinazopatikana katika michezo pamoja na kuwekeza katika sekta hiyo.
Baraza la Michezo la Umoja wa Afrika Kanda ya 4 unajumuisha nchi za Commoros, Djibout, Eritrea, Ethiopia, Kenya, Madagascar, Mauritius, Rwanda, Seychelles, Somalia, Sudani,Sudani Kusini pamoja na Tanzania na Uganda ambao ndiyo wenyeji.