Habari
DC Ndemanga Awataka Waandaaji wa Matamasha Kufungua Milango kwa Wadau Zaidi
Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Mhe. Shaibu Ndemanga, amewataka waandaaji wa Tamasha la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo pamoja na waandaaji wa matamasha mengine nchini kuendelea kufungua milango kwa wadau mbalimbali ili kuongeza ushirikiano katika kuandaa na kuendesha matukio hayo muhimu kwa maendeleo ya sanaa na utamaduni nchini.
Ametoa wito huo Oktoba 31, 2026 wakati akizungumza katika kilele cha Tamasha la 44 la Kimataifa la Sanaa na Utamaduni Bagamoyo lililofanyika katika viwanja vya Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TaSUBa) Bagamoyo, mkoani Pwani, kuanzia Oktoba 28 hadi 31, 2026.
Mhe. Ndemanga amesema ushirikiano wa wadau ni muhimu katika kuhakikisha matamasha yanaendelea kukua na kuwa na tija kwa Taifa, huku akibainisha kuwa changamoto katika maandalizi na uendeshaji wa matukio makubwa kama hayo haziwezi kukosekana.
“Niwaombe waandaaji wa Tamasha hili na matamasha mengine waendelee kufungua milango ili kukaribisha wadau wengi wa kushirikiana nao kuendesha matukio haya muhimu sana kwa Taifa letu,” amesema Mhe. Ndemanga.
Aidha, ameupongeza uongozi, wafanyakazi, wanachuo wa TaSUBa pamoja na kamati zote za maandalizi ya Tamasha hilo kwa juhudi wanazozifanya katika kuhakikisha tamasha hilo linaendelea kufanyika kwa miaka 44 mfululizo, akieleza kuwa mafanikio hayo yanaonesha dhamira ya dhati ya kudumisha na kuendeleza sanaa na utamaduni.
Katika hatua nyingine, Mhe. Ndemanga amewapongeza wasanii wote walioshiriki katika Tamasha hilo, hususan wale waliojitolea kugharamia ushiriki wao wenyewe, akieleza kuwa kitendo hicho ni ishara ya uthubutu, kujitolea na mshikamano katika kukuza sanaa na utamaduni wa Tanzania.
“Karibu wasanii wote wamejigharamia wao wenyewe, hakika huu ni uthubutu wa kiwango cha hali ya juu, nawapongeza na kuwashukuru kwa ushiriki wenu ambao si tu umenitia moyo, bali pia umeonesha mshikamano katika kudumisha na kuendeleza sanaa na utamaduni wetu,” amesisitiza.
Mhe. Ndemanga amewahamasisha wananchi wa Bagamoyo na Watanzania kwa ujumla kujitokeza kwa wingi katika matamasha yajayo ili kuwaunga mkono wasanii na kutambua mchango wao katika kukuza na kuendeleza sanaa nchini.
