Habari
WAJASIRIAMALI WATAKIWA KUONGEZA UBUNIFU
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Ajira na Mahusiano, Mhe. Deus Clement Sangu, amewataka Wajasiriamali nchini Tanzania na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) kuendelea kuongeza ubunifu, ubora na ushindani wa bidhaa zao ili kunufaika na fursa za masoko zinazotokana na ushirikiano wa kikanda.
Waziri Sangu ametoa wito huo Novemba 6, 2026, jijini Kigali, Rwanda, katika Maadhimisho ya Siku ya Tanzania kwenye Maonesho ya 26 ya Jua Kali yanayofanyika nchini humo.
Amesema kuwa, ubunifu ni nyenzo muhimu katika kukuza biashara na kuongeza ushindani wa bidhaa za wajasiriamali katika masoko ya ndani na kimataifa.
“Nimefurahishwa kuona bidhaa mbalimbali kutoka kwa wajasiriamali wetu. Kwa kweli, bidhaa zilizopo zinaonesha kuwa wajasiriamali wetu ni wabunifu na wanaweza kufanya mambo makubwa zaidi kama watapewa fursa. Nawapongeza kwa ubunifu huu, lakini nawashauri muwe wabunifu zaidi kwa kuzingatia kuwa biashara ni ushindani,” amesisitiza Mhe. Sangu.
Amesema, maonesho hayo ni jukwaa muhimu la kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi miongoni mwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kupanua masoko, kukuza biashara na kuongeza fursa za ajira kwa Wananchi.
Ameongeza kuwa maonesho hayo yanafanyika kwa mara ya 26 tangu kuanzishwa kwake mwaka 1999 jijini Arusha, Tanzania, na kwamba mwaka huu yanashirikisha zaidi ya wajasiriamali 2,500 kutoka nchi wanachama wa Jumuiya hiyo, ikilinganishwa na washiriki 2,241 mwaka uliopita.
Aidha, amesema sekta ya ubunifu bado inakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwemo upatikanaji wa mitaji, maeneo ya kufanyia biashara, masoko, elimu ya ujasiriamali na viwango vya ubora wa bidhaa, pamoja na mazingira yasiyo bora na yasiyo na staha ya kufanyia kazi, ambayo ameahidi kuyafanyia kazi kupitia nchi wanachama.
Siku ya Tanzania imepambwa na maonesho ya mavazi ya asili ambapo
Wajasiriamali wa kazi bunifu wa Kitanzania wameonesha mavazi ya Kitenge na Batiki, mikoba ya ngozi, viatu vya ngozi na vyakula vya asili vya jamii ya Tanzania.
