Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO

Habari

KUMBUKUMBU YA KUDUMU KUTEKELEZWA MAZIMBU


Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Serikali ya Afrika Kusini imeanza mchakato wa ujenzi wa Mnara wa Mashujaa katika eneo la Makaburi ya Mashujaa wa Afrika Kusini yaliyopo Mazimbu, mkoani Morogoro, ikiwa ni sehemu ya kuenzi mchango wa mashujaa hao na kudumisha kumbukumbu yao kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika eneo hilo Oktoba 23, 2026, Balozi wa Afrika Kusini nchini Tanzania, Mhe. Noluthando Mayende-Malepe, amesema kuwa, mpango wa kujenga mnara huo unalenga kuhifadhi historia ya mashujaa wa Afrika Kusini waliopigania ukombozi wa taifa hilo, pamoja na kuhakikisha kuwa mchango wao unaendelea kutambuliwa na kukumbukwa.

“Ujenzi wa Mnara hapa Mazimbu ni hatua muhimu ya kuhifadhi historia yetu ya pamoja na kuhakikisha kuwa mchango wa mashujaa wetu waliopigania ukombozi unakumbukwa na vizazi vya sasa na vijavyo, Tunathamini mchango wa Tanzania katika harakati za ukombozi wa Afrika Kusini, na kumbukumbu hii itaendelea kuimarisha urafiki, mshikamano na ushirikiano wa kihistoria kati ya mataifa yetu mawili,” amesema Balozi Mayende-Malepe.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kilombero, Mhe. Dustun Kyobya, akizungumza kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, amesema kuwa ujenzi wa mnara huo ni hatua muhimu katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa kihistoria kati ya Tanzania na Afrika Kusini, pamoja na kuongeza fursa za utalii wa kihistoria na ukombozi katika eneo hilo.

Naye Mkurugenzi wa Utamaduni wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw. Boniface Kadili, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, amesema kuwa, Serikali ya Tanzania tayari imetoa kibali kwa Serikali ya Afrika Kusini kutekeleza mpango huo, ikiwa ni sehemu ya juhudi za pamoja za kuwaenzi mashujaa waliochangia katika harakati za ukombozi wa taifa hilo.

Ameongeza kuwa, Serikali ya Tanzania inaendelea kuboresha maeneo mbalimbali ya kihistoria yanayohusiana na harakati za ukombozi kwa lengo la kuyatunza, kuyaendeleza na kuyatumia kama vivutio vya utalii wa kihistoria na ukombozi. 

Ujenzi wa mnara huo unatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya kuhifadhi historia ya mshikamano na ushirikiano kati ya Tanzania na Afrika Kusini, huku ukiwa ukumbusho wa kudumu wa mchango wa mashujaa wa Afrika Kusini waliopata hifadhi na kuungwa mkono nchini Tanzania wakati wa harakati za kupigania uhuru.

slot gacor