Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO

Habari

MAANDALIZI YA AFCON NA MISS WORLD 2027 YAWE SHIRIKISHI


Watumishi wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo wametakiwa kushirikiana na kutoa mawazo bunifu katika maandalizi ya mashindano ya Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON) 2027 na Miss World 2027 ili kuhakikisha matukio hayo yanafanikiwa na kuipa Tanzania heshima kimataifa.

Wito huo umetolewa  Novemba 17, 2026, na Naibu Katibu Mkuu wa wizara hiyo, Bw. Methusela Ntonda, alipofungua Mkutano wa  wa Baraza la Wafanyakazi wa wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2026/2027, uliofanyika jijini Mwanza.

Ntonda amesema maandalizi ya matukio hayo makubwa ya kimataifa yanahitaji ushirikiano wa watumishi wa Idara na Taasisi zote zilizo chini ya wizara hiyo, akisisitiza kuwa, mafanikio yake hayawezi kupatikana kwa juhudi za idara moja pekee.

Amesema Tanzania itakuwa mwenyeji wa AFCON 2027 kwa kushirikiana na Kenya na Uganda, kuanzia Juni 19 hadi Julai 17, 2027, akiongeza kuwa  imepata heshima ya kuwa mwenyeji wa Miss World 2027.

Alibainisha kuwa maandalizi ya AFCON yanahusisha utekelezaji wa miradi 34 katika maeneo mbalimbali, ikiwamo ujenzi wa viwanja vya michezo na barabara zinazounganisha viwanja hivyo katika miji mwenyeji ya Dar es Salaam na Arusha.

Amesema pamoja na uwekezaji mkubwa unaofanyika, mafanikio ya mashindano hayo yanapaswa kuonekana katika sekta nyingine za uchumi, zikiwamo utalii, usafirishaji, malazi, huduma za chakula, biashara na ajira kwa wananchi.

“AFCON si mashindano ya mpira wa miguu pekee, bali ni fursa ya kimkakati kiuchumi na kijamii inayoweza kunufaisha sekta mbalimbali,” alisema.

Ameongeza kuwa, sekta ya Habari ina wajibu wa kuhakikisha taarifa sahihi kuhusu maandalizi zinafika kwa wananchi kwa wakati, mafanikio yanatangazwa ipasavyo na taarifa potofu zinakabiliwa kupitia njia sahihi za mawasiliano.

Kwa upande wa utamaduni na sanaa, alisema mashindano hayo ni fursa ya kutangaza utajiri wa urithi wa Tanzania kupitia muziki, ngoma, filamu, mavazi na kazi nyingine za sanaa, sambamba na kukuza lugha ya Kiswahili kimataifa.

Aidha, Ntonda amesisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya idara na taasisi za wizara hiyo katika kutekeleza majukumu yao, akitolea mfano wa Bodi ya Filamu na taasisi nyingine zinazohusika na maendeleo ya wasanii, pamoja na ushirikiano wa taasisi za lugha katika kuandaa kamusi za michezo na kupata wakalimani kuelekea AFCON.

Amesisitiza kuwa, mafanikio ya wizara yanategemea pia ubunifu, uadilifu, uwajibikaji na ushirikiano wa watumishi wote kuanzia ngazi za chini hadi uongozi wa juu.


Kwa upande wake, Katibu wa Baraza la Wafanyakazi, Sephania Motela, amesema mkutano huo unalenga kupokea na kujadili taarifa za utekelezaji wa bajeti ya wizara kwa kipindi cha Julai hadi Oktoba 2026, maazimio ya mkutano uliopita na utekelezaji wa miradi ya kimkakati, hususan maandalizi ya AFCON.

Amesema mkutano huo wa siku mbili pia utajadili masuala ya utamaduni na maadili, matumizi ya akili unde kuongeza ufanisi mahali pa kazi pamoja na fursa za uwekezaji kupitia Miss World, huku ukitarajiwa kuhitimishwa kwa maazimio yatakayoweka msingi wa utekelezaji.

Naye Mwenyekiti wa TUGHE, Tawi la Wizara, Nyambeho Magesa, amesema mkutano huo ni sehemu ya utekelezaji wa sheria na mkataba wa mwajiri na chama cha wafanyakazi unaolenga kuimarisha ushirikishwaji wa watumishi katika maamuzi yanayohusu maslahi na mazingira yao ya kazi.

Aidha, mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Ofisa Sanaa, Kemilembe Anatory, amesema kikao hicho kimekuwa muhimu kwa kuwakumbusha watumishi wajibu wao katika maandalizi ya AFCON na Miss World 2027.

slot gacor