Habari
WIZARA YA HABARI KUANZISHA SACCOS KUIMARISHA USTAWI WA WATUMISHI
Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo imeanza mchakato wa kuanzisha Chama cha Akiba na Mikopo (SACCOS) kitakachomilikiwa na watumishi kwa lengo la kuwawezesha kuweka akiba, kupata mikopo kwa masharti nafuu na kuimarisha ustawi wao kiuchumi.
Akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya uanzishaji wa SACCOS hiyo Novemba 3, 2026 Mtumba, jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali Watu wa Wizara hiyo, Bi. Savera Salvatory, amesema chama hicho kitatoa fursa kwa watumishi kuunganisha nguvu zao za kiuchumi kupitia utaratibu wa pamoja wa kuweka akiba na kukopeshana.
Amesema mafunzo hayo yanalenga kuwajengea watumishi uelewa kuhusu taratibu za kisheria, masharti ya uanzishaji, usajili, uongozi na usimamizi wa vyama vya ushirika ili kuhakikisha SACCOS hiyo inaanzishwa kwa misingi imara.
"Mafunzo haya yatatoa fursa ya kujifunza masuala mbalimbali yanayohusu taratibu za kisheria, masharti, usajili, uongozi na usimamizi wa SACCOS ili kupata uelewa wa pamoja wa kuanzisha SACCOS yetu," amesisitiza Bi. Savera.
Mafunzo hayo yametolewa na viongozi wa vyama vya ushirika kutoka Ofisi ya Jiji la Dodoma, yakijikita katika masuala ya uanzishaji na usimamizi wa vyama hivyo.
