Habari
UBUNIFU WA TANZANIA KUIPAMBA JUAKALI RWANDA
Wajasiriamali takriban 350 wa Sekta ya Ubunifu kutoka Tanzania wapo nchini Rwanda kushiriki Maonesho ya 26 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki maarufu kama Juakali.
Wakizungumza katika maonesho hayo tarehe 2 Novemba 2026, wamesema maonesho hayo ni chachu kubwa ya kutangaza kazi za sanaa bunifu za Kitanzania katika soko la kimataifa.
Mmoja wa washiriki, Paul Onesmo, ambaye ni mbunifu wa bidhaa za ngozi amesema kupitia maonesho hayo wamepata nafasi ya kuonesha kuwa sanaa bunifu ya Tanzania ni ajira na biashara inayoweza kushindana kimataifa.
Tunaonesha dunia kuwa ngozi ya Tanzania inaweza kutengeneza mikoba, viatu na mikanda ya kisasa kabisa. Wateja kutoka Kenya, Uganda na Rwanda wanavutiwa na ubunifu wetu," amesema Paul.
Kwa upande wake Janeth Geofrey ambaye ni mjasiriamali wa sekta ya sanaa bunifu inayohusiana na vyakula vya asili na mapishi ya Kitanzania, amesema kupitia maonesho hayo wamejifunza namna ya kufungasha bidhaa zao kwa ubunifu zaidi ili ziweze kufikia masoko ya kimataifa.
"Maonesho haya yamekuwa darasa kubwa la kujifunza teknolojia mpya za ubunifu, mitindo ya soko la Afrika Mashariki, na namna ya kutumia mitandao ya kijamii kutangaza kazi za sanaa" amesema Janeth.
Wamesema ushiriki wao umewasaidia kupata kipato cha moja kwa moja kupitia mauzo na oda wanazopata, huku wakifungua fursa za ushirikiano na wanunuzi na wasambazaji kutoka nchi mbalimbali za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Katika hatua nyingine, wameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwaunga mkono wasanii bunifu kwa kuwapatia fursa zaidi za kushiriki maonesho ya ndani na nje ya nchi, pamoja na mafunzo ya namna ya kulinda kazi zao, kimiliki na kuziuza kwa ubora unaokubalika kimataifa.
