Habari
TANZANIA YAVUMA KIGALI
Waziri Mkuu wa Rwanda, Mhe. Dkt. Justin Nsengiyumva, amezipongeza bidhaa za ubunifu kutoka kwa wajasiriamali wa Sekta ya Sanaa Bunifu wa Tanzania na kutoa wito kwa wabunifu hao kuzingatia masoko ya nje ya nchi ili kuinua biashara zao.
Dkt. Nsengiyumva amesema hayo alipotembelea banda la wajasiriamali kutoka Tanzania Bara na Zanzibar, mara baada ya kuzindua rasmi Maonyesho ya 26 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati ya Afrika Mashariki - Nguvu Kazi maarufu Jua Kali, yanayoendelea katika Viwanja vya Gikondo nchini Rwanda, Novemba 3, 2026.
Amesema ubunifu uliooneshwa kwenye bidhaa hizo ni mfano wa kuigwa na Jumuiya ya Afrika Mashariki, huku akipongeza jitihada za wajasiriamali hao kwa kutumia vipaji vya asili na teknolojia ya kisasa kuzalisha bidhaa zenye ubora unaokidhi soko la kimataifa.
Miongoni mwa bidhaa za ubunifu kutoka Tanzania ni Mavazi ya vitenge na batiki, bidhaa za ngozi kama vile viatu, mabegi, mikoba na mikanda, bidhaa za urembo wa asili, vyakula vya asili, bidhaa za uchongaji pamoja na picha za uchoraji.
