Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO

Habari

TANZANIA KUWA MWENYEJI WA MAONESHO YA JUA KALI 2027


Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inatarajiwa kuwa mwenyeji wa Maonesho ya 27 ya Wajasiriamali Wadogo na wa Kati wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, yanayojulikana kama Jua Kali / Nguvu Kazi, mwaka 2027.

Akitangaza uteuzi huo jana Novemba 8, 2026, Jijini Kigali, Naibu Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki anayeshughulikia Forodha, Biashara na Fedha, Bi. Annette Mutaawe, amesema Tanzania imeteuliwa kuandaa maonesho hayo kufuatia kukamilika kwa mzunguko wa nchi zote nane wanachama.

Bi. Mutaawe, pamoja na tangazo hilo, alikabidhi bendera ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kwa mwakilishi wa Serikali ya Tanzania kuonyesha utayari wa kuandaa na kuratibu maonesho hayo yenye lengo la kukuza fursa za biashara, masoko na kubadilishana teknolojia miongoni mwa wajasiriamali wadogo na wa kati.

Naibu Katibu Mkuu huyo ameongeza kuwa Sekretariati ya Afrika Mashariki itaendelea kutafuta suluhu ya changamoto zinazowakabili wajasiriamali, ikiwemo kuondoa vikwazo vya usafirishaji mipakani, huduma za forodha, teknolojia duni ya usindikaji na uongezaji thamani ya bidhaa.

Akizungumza baada ya kukabidhiwa bendera hiyo, Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Ukuzaji Ajira kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira na Mahusiano, Bi. Alana Nchimbi, amesema Tanzania imepokea dhamana hiyo na itafanya maandalizi ya kutosha.

"Tunatambua kuwa jukumu hili si heshima tu kwa Tanzania, bali ni dhamana ya kuendeleza ajenda ya pamoja ya kukuza biashara, uwekezaji na maendeleo ya kiuchumi ndani ya Jumuiya yetu," amesisitiza Alana.

Katika maonesho ya mwaka huu yaliyofanyika Kigali, Tanzania iliwakilishwa na wajasiriamali 374 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo wajasiriamali wanne waliibuka washindi kati ya makundi sita yaliyoshindanishwa.

slot gacor