Habari
UMITASHUMTA YAZIDI KUZALISHA VIPAJI, SERIKALI YAONGEZA UWEKEZAJI
Serikali imetenga Shilingi bilioni 15 katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kukamilisha ujenzi wa Akademia ya Taifa ya Michezo iliyopo Chuo cha Maendeleo ya Michezo Malya, hatua inayolenga kuimarisha mfumo wa kuibua na kukuza vipaji vinavyopatikana kupitia mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA.
Akizungumza wakati wa kufunga mashindano ya Umoja wa Michezo na Taaluma kwa Shule za Msingi Tanzania (UMITASHUMTA) 2026 yaliyofanyika mkoani Iringa Juni 17 2026, Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaendelea kuwekeza kwa nguvu katika sekta ya michezo na sanaa kutokana na mchango wake katika ajira, afya na ushindani wa kimataifa.
Mhe. Mwinjuma amesema kuwa akademia hiyo itakuwa na uwezo wa kupokea na kuendeleza vipaji vinavyogunduliwa katika mashindano ya shule, ili kuandaa kizazi cha wanamichezo watakaoliwakilisha taifa katika mashindano mbalimbali ya kimataifa.
Mwinjuma ameongeza kuwa mafanikio ya hivi karibuni ya timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti Boys, yameonyesha umuhimu wa kuendelea kuwekeza kwenye michezo ya shule, akibainisha kuwa wachezaji wasiopungua watano wa kikosi hicho, akiwemo golikipa namba moja, walitokana na mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA.
Aidha, Mhe. Mwinjuma amesema mashindano hayo ni msingi muhimu wa kuandaa wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Afrika Mashariki (FEASSSA) yatakayofanyika Agosti mwaka huu mkoani Morogoro, huku akiwataka wanamichezo watakaochaguliwa kuitangaza vyema Tanzania.
