Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO

Habari

KONGAMANO LA VIJANA NA UBUNIFU LATOA MWELEKEO MPYA KWA VIJANA


Wakati shamrashamra za Tamasha la Utamaduni la BULABO zikiendelea kuteka hisia za wakazi wa Mkoa wa Mwanza, ambapo mamia ya vijana wamejitokeza kushiriki Kongamano la Vijana na Ubunifu lililokuwa sehemu ya matukio makubwa ya siku ya tano ya tamasha hilo.

Hayo yamejiri leo Juni 11, 2026 ambapo Zaidi ya washiriki 863 kutoka vyuo mbalimbali vya Mkoa wa Mwanza, ikiwemo Chuo cha Mtakatifu Augustino Tanzania (SAUT), Chuo cha Mipango na taasisi nyingine za elimu ya juu, walihudhuria kongamano hilo lililolenga kuwajengea vijana uelewa kuhusu nafasi yao katika kulinda na kuendeleza utamaduni wa Tanzania.

Katika Kongamano hilo Washiriki walipata elimu kuhusu umuhimu wa utamaduni wa Kitanzania kwa kizazi cha sasa, namna ya kulinda maadili ya taifa, kuhifadhi lugha ya Kiswahili pamoja na kutumia mila na desturi kama msingi wa kujenga jamii bora.

Aidha, vijana walijifunza pia kuhusu athari za utandawazi na matumizi ya mitandao ya kijamii kwa utamaduni wa vijana wa Kitanzania, huku wakihimizwa kutumia teknolojia na ubunifu kama nyenzo za kutangaza utamaduni wa nchi badala ya kuupoteza. Vilevile mada kuhusu fursa za kiuchumi zinazotolewa na Serikali kupitia sekta ya utamaduni na sanaa iliwapa mwanga vijana juu ya namna wanavyoweza kujiajiri na kujiongezea kipato kupitia vipaji, ubunifu na shughuli za kiutamaduni.

Kongamano hilo limeonekana kuwa moja ya matukio yenye mvuto mkubwa ndani ya Tamasha la BULABO mwaka huu, likiunganisha elimu, ubunifu na utamaduni katika jukwaa moja. Wakati tamasha hilo likielekea kilele chake Juni 14, 2026 katika Uwanja wa Red Cross Kisesa, wananchi wanaendelea kufurika kushuhudia burudani, maonesho na shughuli mbalimbali zinazodhihirisha utajiri wa tamaduni za Tanzania.

slot gacor