Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO

Habari

NAIBU WAZIRI MWINJUMA AIPONGEZA GSM FOUNDATION NA YANGA SC KWA KLINIKI YA KUSAKA VIPAJI


 

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma, amepongeza uongozi wa GSM Foundation pamoja na Yanga SC kwa kuanzisha kliniki ya soka yenye lengo la kusaka na kuendeleza vipaji vya vijana wadogo huku wakisimamiwa pia katika masuala ya elimu.

Mhe. Mwinjuma amesema hayo leo tarehe 8 Machi, 2026 katika Uwanja wa Gymkhana, jijini Dar es Salaam, alipokuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa kliniki hiyo ya soka inayolenga kukuza vipaji vya watoto na vijana.

Amesema hatua ya taasisi ya GSM Foundation kwa kushirikiana na Yanga SC kuandaa na kusimamia mpango huo ni muhimu katika kuibua vipaji vipya vya soka nchini sambamba na kuhakikisha vijana hao wanapata mwongozo mzuri wa kitaaluma.

Aidha, Mhe. Mwinjuma ameeleza kuwa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuunga mkono jitihada za sekta binafsi zinazochangia maendeleo ya michezo nchini.

Pia amesisitiza kuwa serikali itaendelea kuweka mazingira rafiki ya kisera pamoja na kuwekeza katika ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya michezo ikiwemo viwanja ili kukuza sekta hiyo.

Ikumbukwe kuwa mwaka 2027, Tanzania ni miongoni mwa mataifa yatakayoshiriki kuandaa mashindano ya AFCON, kwa kushirikiana na nchi za Kenya na Uganda, jambo linaloendelea kuchochea maendeleo ya michezo na miundombinu yake nchini.