Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO

Habari

NAIBU WAZIRI MWINJUMA APONGEZA PBZ KUFIKISHA HUDUMA TANGA.


Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Hamis Mwinjuma ametoa pongezi kwa Benki ya PBZ (Ikhlas) kwa kufikisha huduma zake mkoa wa Tanga.

Mhe. Mwinjuma ametoa pongezi hizo, Juni 3, 2026 alipozindua tawi jipya la Benki hiyo ya Watu wa Zanzibar (PBZ Ikhlas) katila Mkoa wa Tanga, ambao ulienda  sambamba na Maadhimisho ya miaka 60 tangu kuanzishwa kwa benki hiyo nchini mwaka 1966.

Akizungumza  katika uzinduzi huo, Mhe. Mwinjuma alisema, hatua hiyo ni kielelezo tosha cha uaminifu na sifa ya Muungano wa Tanzania bara na Zanzibar, ambao umepanua  wigo wa huduma kupitia mfumo wa PBZ Ikhlas. 

"Ufanisi huu mkubwa wa PBZ unaenda sambamba na maono ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, na Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambao kwa pamoja wanasimamia mageuzi ya kiuchumi yanayojenga soko shindani kupitia matumizi ya teknolojia ya kisasa ya kibenki," alisisitiza Mhe. Mwinjuma.

Ameongeza kuwa, Mkoa wa Tanga una umuhimu mkubwa wa kimkakati kupitia miradi mikubwa ambayo Serikali ya Awamu ya Sita imewekeza kwenye miundombinu ya bandari, barabara, reli na nishati, jambo linalofungua milango kwa ustawi wa sekta binafsi, akitoa wito kwa wananchi kutumia huduma za PBZ Ikhlas kuongeza akiba, kupata mikopo, na kuwekeza ili kukuza uchumi wao wa kila siku.

Naye Meneja Masoko na Kuendeleza Biashara wa PBZ, Seif Suleiman, amesema ujio wa tawi hilo unalenga kuchochea fursa za kiuchumi kwa sababu Tanga ni lango kuu linalokua kwa kasi na linapakana na Jiji la Mombasa, nchini Kenya.

"Tunajivunia miaka 60 ya uaminifu nchini. Uamuzi wa kuleta PBZ Ikhlas Tanga umechochewa na fursa za kiuchumi na mshabihiano mkubwa wa kitamaduni kati ya Tanga na Zanzibar. Benki hii si ya Waislamu pekee, ni chombo cha watu wote," alisema Suleiman.

Suleiman ameongeza kuwa kwa sasa PBZ ni benki ya sita kwa ukubwa nchini ikiwa na vituo na matawi ya kutolewa huduma yapatayo 50 Bara na Visiwani. Katika hatua hiyo, uongozi ulimshukuru Muasisi Marehemu Abeid Amani Karume kwa maono yake yaliyowezesha taasisi hiyo kuzaliwa.

Katika hatua nyingine, uzinduzi huo ulishuhudia utiaji saini wa makubaliano ya kimasomo kati ya PBZ na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB). Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Dkt. Bill Kiwia, alithibitisha kusainiwa kwa akaunti maalum ya dharura ya elimu itakayosaidia vijana kupata ufadhili wa masomo kupitia benki hiyo kwa misingi isiyo na riba.

slot gacor