Tanzania emblem

Jamhuri ya Muungano wa Tanzania

WIZARA YA HABARI, UTAMADUNI, SANAA NA MICHEZO

Habari

NAIBU KATIBU MKUU NTONDA AWATAKA WAJUMBE WA BARAZA KUWA WAWAKILISHI WAZURI


 

Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Ndg. Methusela Ntonda, amewataka wajumbe wa Baraza la Wafanyakazi kutekeleza wajibu wao kwa ufanisi na uadilifu ili kupata matokeo yenye tija kwa niaba ya watumishi wa Wizara hiyo. 

Ametoa wito huo leo Machi 04, 2026, wakati akizindua Baraza hilo katika ukumbi wa Wizara, Mtumba jijini Dodoma.

Ntonda amesema kuwa wajumbe hao wamechaguliwa kwa niaba ya wafanyakazi, hivyo wanapaswa kuwa wawakilishi wazuri ili kuchochea ufanisi wa Watumishi mahali pa kazi.

Aidha, alitaja mafanikio ambayo wizara imepata kwa mwaka wa fedha 2025/26 kuwa ni Kiswahili kutambuliwa na UNESCO kama miongoni mwa Lugha zake rasmi, Mwezi Novemba 2025, Muziki wa Singeli kutambulika kama sehemu ya Urithi wa dunia, kuelemisha Umma kuhusu historia ya Ukombozi wa Bara la Afrika.

Pia katika Michezo Ntonda ametaja Kuwa Uwenyeji wa CHAN 2025, Ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya Viwanja vya Mpira na Mazoezi, mafanikio ya timu za Taifa za michezo na kueleza kuwa mafanikio hayo ni sehemu ya maandalizi ya AFCON 2027 ambapo Tanzania ni mwenyeji wa michuano hiyo.

Naye Mkurugenzi wa Utawala na Usimamizi wa Rasilimali watu, Bi. Savera Salvatory Kazaura amewapongeza viongozi wa Baraza na wajumbe waliochaguliwa sambamba na kuwataka Menejimenti na Wakuu wa Wizara hiyo kuwapa ushirikiano ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa wepesi.

Katika mkutano huo, taarifa  mbalimbali ziliwasilishwa  ikiwemo Mapitio ya Bajeti ya mwaka wa Fedha 25/26 na Maoteo ya bajeti kwa mwaka wa fedha 26/27 pamoja na uchaguzi wa viongozi wa Baraza.