Habari
MICHEZO YAIMARISHA USHIRIKIANO TANZANIA NA CHINA
Sekta ya michezo imekua daraja la kuimarisha urafiki, mshikamano na ushirikiano kati ya Tanzania na China kupitia ushirikiano kwenye sekta hiyo ikiwemo uwekezaji katika miundombinu, biashara na elimu.
Hayo yamesemwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa, leo Agosti 1, 2026, wakati akifungua Mashindano ya 13 ya Mpira wa Kikapu ya Chama cha Wafanyabiashara wa China (Tanzania) katika viwanja vya Don Bosco, Oysterbay, Dar es Salaam.
Msigwa amesema, Tanzania na China zina ushirikiano wa muda mrefu, ambao umeleta maendeleo kwa nchi hizo, huku akiishukuru Serikali ya China kwa mchango wake katika sekta ya michezo nchini na kuhimiza uwekezaji zaidi kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.
Kwa upande wake Balozi wa China hapa Bi. Chen Mingjian, alisema michezo inaendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria kati ya Tanzania na China, huku Mwenyekiti wa Chama cha Wafanyabiashara wa China nchini Tanzania, Jiang Yuntao, akiishukuru Serikali ya Tanzania na Ubalozi wa China kwa kuendelea kuwezesha kufanyika kwa mashindano hayo kila mwaka.
Mashindano hayo yameanza Agosti 1 hadi 8, 2026 na yanasimamiwa na Chama cha Mpira wa Kikapu Tanzania (TBF) kwa kuzingatia kanuni za FIBA ambapo yanakutanisha Kampuni mbalimbali za Kichina zinazofanya shughuli zake hapa nchini.
