Habari
BALOZI WA TANZANIA UFARANSA AONGOZA MKUTANO WA NCHI ZA AFRIKA KUJIANDAA NA KIKAO CHA KAMATI YA URITHI WA DUNIA YA UNESCO
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika UNESCO, Mhe. Saidi Othman Yakubu, ameongoza Mkutano wa 9 wa Nchi Wanachama wa Afrika katika Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO uliofanyika jijini Dakar, Senegal.
Mkutano huo uliwakutanisha wajumbe kutoka Senegal, Angola, Kenya, Namibia, Comoro, Togo, Gambia, Uganda, Tanzania, Afrika Kusini, Malawi na Tunisia kwa lengo la kuratibu misimamo ya pamoja ya Afrika kuelekea Kikao cha 48 cha Kamati ya Urithi wa Dunia ya UNESCO kitakachofanyika Busan, Jamhuri ya Korea.
Akiongoza mkutano huo, Mhe. Yakubu alisisitiza umuhimu wa nchi za Afrika kuendelea kushirikiana kwa karibu ili kulinda, kuhifadhi na kuendeleza urithi wa asili na wa utamaduni wa bara hilo pamoja na kuhakikisha sauti ya Afrika inasikika kwa nguvu katika majukwaa ya kimataifa yanayojadili masuala ya urithi wa dunia.
Mkutano huo ulihudhuriwa pia na Mkuu wa Kundi la Afrika katika UNESCO na Mwakilishi wa Kudumu wa Senegal katika UNESCO, Mhe. Balozi Pierre Faye, pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Urithi wa Dunia wa Afrika (African World Heritage Fund - AWHF), Dkt. Albino Jopela.
Katika mjadala huo, wajumbe walijadili kwa kina masuala yanayohusu maeneo ya urithi wa dunia barani Afrika, ikiwemo hali ya uhifadhi wa maeneo yaliyopo katika Orodha ya Urithi wa Dunia, mikakati ya kuondoa maeneo yaliyo katika hatari, pamoja na namna ya kuongeza uwakilishi wa maeneo ya Afrika katika Orodha ya Urithi wa Dunia ya UNESCO.
Aidha, wajumbe walibadilishana uzoefu kuhusu changamoto zinazoikabili sekta ya urithi wa dunia barani Afrika, ikiwemo athari za mabadiliko ya tabianchi, ongezeko la shughuli za kibinadamu katika maeneo ya urithi, upungufu wa rasilimali za uhifadhi na umuhimu wa kuimarisha ushiriki wa jamii katika kulinda urithi huo.
Mkutano huo pia ulijadili fursa za kuongeza ushirikiano kati ya nchi za Afrika, UNESCO na wadau mbalimbali wa maendeleo ili kuhakikisha kuwa urithi wa bara la Afrika unalindwa, unatunzwa na kutumika kama nyenzo ya maendeleo endelevu, utalii, ajira na ustawi wa jamii.
Mhe. Yakubu alieleza kuwa Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi nyingine za Afrika katika kuendeleza ajenda za urithi wa dunia na kuhakikisha maslahi ya bara yanapewa kipaumbele katika mijadala na maamuzi yanayofanyika ndani ya UNESCO.
Uenyekiti wa Tanzania katika mkutano huo unaendelea kudhihirisha nafasi muhimu ya nchi katika kukuza ushirikiano wa kimataifa, kuimarisha diplomasia ya utamaduni na kuendeleza ajenda za Afrika ndani ya UNESCO na taasisi zake mbalimbali.
Mkutano huo umefanyika sambamba na maadhimisho ya miaka 20 ya Mfuko wa Urithi wa Dunia wa Afrika (AWHF), taasisi ya Afrika iliyoanzishwa kusaidia juhudi za uhifadhi, usimamizi na maendeleo ya maeneo ya urithi wa dunia barani Afrika.
