Habari
BALOZI MWADINI ATETA NA WATAALAM WA WIZARA KUFANIKISHA KONGAMANO LA KISWAHILI UFARANSA
Balozi wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania nchini Ufaransa, Mhe. Jabir Mwadini, amekutana na wataalamu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo pamoja na wadau wa sekta mbalimbali kujadili maandalizi ya Kongamano la Kimataifa la Kiswahili litakalofanyika kuanzia tarehe 27–30 Aprili 2026 jijini Paris.
Kikao hicho kilichofanyika jijini Dar es Salaam, kililenga kuweka mikakati madhubuti ya kufanikisha kongamano hilo, ambalo linatarajiwa kuwa jukwaa muhimu la kukuza na kueneza lugha ya Kiswahili kimataifa.
Katika mazungumzo hayo, Mhe. Mwadini alisisitiza umuhimu wa kushirikisha sekta binafsi pamoja na Watanzania wa Diaspora ili kuhakikisha kongamano hilo linafanikiwa na kufikia malengo yake, ikiwemo kuitangaza Tanzania kimataifa na kuimarisha diplomasia ya kiuchumi. Alieleza kuwa ubalozi uko tayari kutoa ushirikiano wa karibu katika maandalizi na utekelezaji wa tukio hilo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Utamaduni, Bw. Boniface Kadili, alimshukuru Balozi kwa ushirikiano wake endelevu na Wizara pamoja na taasisi mbalimbali katika maandalizi ya kongamano hilo. Alibainisha kuwa lengo kuu ni kukuza na kuendeleza lugha adhimu ya Kiswahili kimataifa sambamba na kuchochea maendeleo katika sekta za utalii, elimu, biashara na uwekezaji.
Aidha, Bw. Kadili aliipongeza ubalozi kwa juhudi za kukipenyeza Kiswahili katika Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, ambapo kwa sasa Kiswahili ni miongoni mwa lugha rasmi zinazotumika katika Mikutano Mikuu ya shirika hilo.
