Habari
KATIBU MKUU MSIGWA AONESHA UMAHIRI WAKE KATIKA MICHEZO
Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Msemaji Mkuu wa Serikali, Gerson Msigwa ameendelea kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika michezo kwa kushiriki moja kwa moja hususani mpira wa miguu.
Msigwa amekua miongoni mwa viongozi wanaonesha ushiriki wa moja kwa moja katika michezo, ambapo leo Juni 20, 2026 ameshiriki CRDB Bank Grand Bunge Bonanza 2026 katika uwanja wa Jamhuri Dodoma.
Katika mchezo wa mpira wa miguu uliowakutanisha Mabalozi wa mataifa mbalimbali wanaowakilisha nchi zao nchini Tanzania ambao wameungana na Wizara ya Habari dhidi ya timu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, timu ya Mabalozi imeibuka na ushindi wa goli 5- 4 kwa mikwaju ya penati baada ya kutoka sare ya 1-1 katika muda wa kawaida wa mchezo.
Mara baada ya mchezo huo, Msigwa amesema kuwa mbali na ushindani wa uwanjani mchezo huo umeendelea kuonesha nafasi ya michezo kama nyenzo muhimu ya kuimarisha diplomasia, kujenga urafiki na kuendeleza ushirikiano kati ya Tanzania na Jumuiya ya kimataifa.
