Habari
TANZANIA YAPONGEZA CHINA NA URUSI KWA KUENDELEZA USHIRIKIANO
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe. Paul Makonda ametoa pongezi kwa Nchi ya China na Urusi kwa kuendelea kushirikiana ambapo ushirikiano huo umetimiza miaka 25.
Mhe. Makonda ametoa pongezi hizo tarehe 24 Juni, 2026 alipokuwa mgeni rasmi katika sherehe ya ushirikiano huo jijini Dar es Salaam, akisema Tanzania itaendelea kudumisha ushirikiano na China na Urusi katika nyanja mbalimbali ikiwemo habari, utamaduni, sanaa na michezo.
"Tanzania inayapongeza Mataifa yote mawili kwa kuonesha umuhimu wa ushirikiano wa miaka 25 ambao unachagiza zaidi maendeleo. Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi hizi katika kuhakikisha urafiki ustawi wa raia wa Mataifa yote matatu unazidi kuimarika katika nyanja mbalimbali" amesisitiza Mhe. Makonda.
Katika kuadhimisha miaka hiyo ya ushirikiano mataifa hayo yaliandaa filamu ya pamoja inayoitwa Red Silk (2025), iliyowakutanisha pamoja Waigizaji wa Mataifa yote mawili.
Filamu hiyo imeoneshwa katika Jumba la Urusi Jijini Dar es salaam jana June 24,2026 ikiwa ni sehemu ya kuadhimisha miaka 25 ya ushirikiano wa urafiki mwema kati ya China na Urusi
Sherehe za ushirikiano huo, zimeandaliwa na ubalozi wa China nchini Tanzania na Ubalozi wa Urusi nchini Tanzania wakiongozwa na Balozi wa China nchini Tanzania, Chen Mingjian na Balozi wa Urusi nchini Tanzania, Andrey Avetisyan
