Habari
TANZANIA YAINGIA KWENYE HISTORIA YA KUANDAA MISS WORLD AFRIKA
Tanzania imeandika historia mpya katika tasnia ya urembo duniani baada ya kuwa nchi ya pili Barani Afrika kuandaa mashindano ya 74 ya "Miss World' na kuwa ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ikitanguliwa na Afrika Kusini ambayo iliandaa mashindano hayo kwa mara ya mwisho mwaka 2009.
Kauli hiyo imetolewa Aprili 20, 2026 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda wakati wa hafla ya utiaji saini wa mkataba wa Tanzania kuwa mwenyeji wa mashindano ya Miss World 2027, tukio linalotarajiwa kuiweka Tanzania katika nafasi mpya kimataifa.
Akizungumza katika hafla hiyo, amesema hatua hiyo ni ya kihistoria tangu kuanzishwa kwa mashindano hayo mwaka 1951. “Tangu kuanzishwa kwa Miss World mwaka 1951, nchi mbalimbali zimekuwa zikiandaa mashindano hayo, ikiwemo Uingereza, China na Marekani ambapo katika Bara la Afrika wa ni Afrika Kusini pekee iliyowahi kuandaa.
Ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo itaendelea kukuza tasnia ya urembo nchini na kuhimiza wadau kuanzisha majukwaa mapya ya kuibua vipaji.
“Wizara iko tayari kushirikiana na wadau wote wenye mawazo mapya katika tasnia ya urembo ili kuongeza ushindani chanya na kuitangaza Tanzania kimataifa,” amesema Mhe. Makonda.
Mhe. Makonda amebainisha kuwa mafanikio hayo yamechangiwa kwa kiasi kikubwa na juhudi za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, katika kuitangaza nchi kimataifa pamoja na kuimarisha umoja wa kitaifa.
Mashindano hayo yanatarajiwa kufanyika mwaka 2027, yakihusisha washiriki kutoka zaidi ya nchi 130 na kuvutia zaidi ya wageni 20,000, jambo linalotarajiwa kuongeza fursa za kiuchumi na kukuza sekta ya utalii nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti na Mtendaji Mkuu wa Miss World, Julia Morley amesema ujio wa mashindano hayo ni fahari kubwa kwa Tanzania na yataifanya Tanzania iwe sehemu ya historia muhimu duniani.
