Habari
SERIKALI KUIMARISHA UWEZO WA WALIMU WA MICHEZO
Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Paul Makonda, amesema Serikali inaendelea kuweka mikakati ya kuboresha elimu ya michezo, pamoja na kuinua uwezo wa walimu wa fani hiyo hapa nchini, ili kuhakikisha wanafunzi wanapata maarifa bora kwa maendeleo ya vipaji vyao.
Akizungumza katika hafla ya usiku wa Tuzo kwa Wanamichezo zilizoandaliwa na Baraza la Michezo la Taifa (BMT) tarehe 9 Mei, 2026, Mhe. Makonda amesema, kuna umuhimu wa kuendelea kuwajengea walimu uwezo kupitia programu maalum za mafunzo ili waendane na mahitaji ya sasa.
Ameeleza kuwa, hatua hiyo itasaidia walimu kuelewa vizuri mbinu za ufundishaji pamoja na kuwasaidia wanafunzi kutambua vipaji vyao katika michezo mapema.
"Serikali inalenga kuhakikisha walimu wanaopata nafasi ya kufundisha michezo katika shule zetu wanakuwa na sifa na uelewa unaotakiwa ili kuongeza ubora wa elimu ya michezo.Tunaendelea kuboresha mazingira bora ya kazi, pamoja na motisha kwa walimu zitakazowawezesha kufanya kazi kwa bidii" alisema Mhe. Makonda.
Ameongeza kuwa, Serikali itaendelea kushirikiana na jamii pamoja na wadau mbalimbali ili kuhakikisha sekta ya michezo inazidi kuimarika na kutoa wataalamu wenye ushindani na ubunifu.
